Matthew 27

1Muda wa asubuhi ulipofika, wakuu wote wa makuhani na wazee wa watu walikula njama dhidi ya Yesu wapate kumuua. 2Walimfunga, walimwongoza, na kumfikisha kwa Liwali Pilato.

3Kisha wakati Yuda, ambaye alikuwa amemsaliti, aliona kwamba Yesu amekwisha kuhukumiwa, alijuta na kurudisha vipande thelathini vya fedha kwa mkuu wa makuhani na wazee, 4na akasema, “Nimefanya dhambi kwa kuisaliti damu isiyo na hatia.” Lakini wakajibu, “Inatuhusu nini sisi? Yaangalie hayo mwenyewe.” 5Kisha alivirusha chini vile vipande vya fedha katika hekalu, na kuondoka zake na kujinyonga mwenyewe.

6Mkuu wa makuhani alivichukua vile vipande vya fedha na kusema, “Si halali kuiweka fedha hii katika hazina, kwa sababu ni gharama ya damu.” 7Walijadiliana kwa pamoja na fedha ikatumika kununulia shamba la mfinyazi la kuzika wageni. 8Kwa sababu hii shamba hilo limekuwa likiitwa, “Shamba la damu” hadi leo hii.

9Kisha lile neno lililokuwa limenenwa na nabii Yeremia lilitimia, kusema, “Walitwaa vipande thelathini vya fedha, gharama iliyopangwa na watu wa Israel kwa ajili yake, 10na waliitumia kwa shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyokuwa amenielekeza.”

11Sasa Yesu alisimama mbele ya liwali, na liwali akamwuliza, “Je! Wewe ni mfalme wa Wayahudi?” Yesu alimjibu, “Wewe wasema hivyo.” 12Lakini wakati aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu chochote. 13Kisha Pilato alimwambia, “Hujayasikia mashitaka yote dhidi yako?” 14Lakini hakumjibu hata neno moja, hivyo liwali alijawa na mshangao.

15Sasa katika sikukuu ilikuwa desturi ya liwali kumfungua mfungwa mmoja anayechaguliwa na umati. 16Wakati huo walikuwa na mfungwa sugu jina lake Baraba.

17Hivyo wakati walipokuwa wamekusanyika pamoja, Pilato aliwauliza, “Ni nani mnataka tumfungue kwa ajili yenu?” Baraba au Yesu anayeitwa Kristo?” 18Kwa sababu alijua kwamba wamekwisha kumkamata kwa sababu ya chuki. 19Wakati alipokuwa akiketi kwenye kiti chake cha hukumu, mke wake alimtumia neno na kusema, “Usitende jambo lolote kwa mtu huyo asiye na hatia. Kwani nimeteswa mno hata leo katika ndoto kwa sababu yake.”

20Ndipo wakuu wa makuhani na wazee waliwashawishi makutano wamwombe Baraba, na Yesu auawe. 21Liwali aliwauliza, “Ni yupi kati ya wawili mnataka mimi nimwachie kwenu?” Walisema, “Baraba.” 22Pilato akawaambia, “Nimtendee nini Yesu anayeitwa Kristo?” Wote wakajibu, “Msulibishe”

23Naye akasema, “Kwa nini, ni kosa gani ametenda?” Lakini walizidi kupaza sauti hata juu mno, “Msulibishe.” 24Hivyo wakati Pilato alipoona hawezi kufanya lolote, lakini badala yake vurugu zilikuwa zimeanza, alitwaa maji akanawa mikono yake mbele ya umati, na kusema, “Mimi sina hatia juu ya damu ya mtu huyu asiye na hatia. Yaangalieni haya wenyewe.”

25Watu wote wakasema, “Damu yake iwe juu yetu na watoto wetu.” 26Kisha akamfungulia Baraba kwao, lakini alimpiga mijeredi Yesu na kumkabidhi kwao kwenda kusulibiwa.

27Kisha askari wa liwali wakamchukua Yesu mpaka Praitorio na kundi kubwa la maaskari wote wakamkusanyika. 28Wakamvua nguo zake na kumvika kanzu ya rangi nyekundu. 29Kisha wakatengeneza taji ya miiba na kuiweka juu ya kichwa chake, na walimwekea mwanzi katika mkono wake wa kuume. Walipiga magoti mbele yake na kumkejeri, wakisema, “Salamu, Mfalme wa Wayahudi?”

30Na walimtemea mate, na walitwaa mwanzi na kumpiga kichwani. 31Wakati walipokuwa wakimkejeri, walimvua ile kanzu na kumvika nguo zake, na kumwongoza kwenda kumsulibisha.

32Walipotoka nje, walimwona mtu kutoka Krene jina lake Simeoni, ambaye walimlazimisha kwenda nao ili apate kuubeba msalaba wake. 33Walipofika mahali paitwapo Galigotha, maana yake, “Eneo la fuvu la Kichwa.” 34Walimpa siki iliyochanganywa na nyongo anywe. Lakini alipoionja, hakuweza kuinywa.

35Wakati walipokuwa wamemsulibisha, waligawana mavazi yake kwa kupiga kura. 36Na waliketi na kumwangalia. 37Juu ya kichwa chake waliweka mashitaka dhidi yake yakisomeka, “Huyu ni Yesu, mfalme wa Wayahudi.”

38Wanyang’anyi wawili walisulibiwa pamoja naye, mmoja upande wa kulia wake na mwingine wa kushoto. 39Wale waliokuwa wakipita walimdhihaki, wakitikisa vichwa vyao 40na kusema, “Wewe uliyekuwa unataka kuliharibu hekalu na kulijenga katika siku tatu, jiokoe mwenyewe! Kama ni Mwana wa Mungu, shuka chini utoke msalabani!”

41Katika hali ile ile wakuu wa makuhani walikuwa wakimkashifu, pamoja na waandishi na wazee, na kusema, 42“Aliokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni Mfalme wa Wayahudi. Na ashuke chini toka msalabani, ndipo tutakapomwamini.

43Alimtumaini Mungu. Acha Mungu amwokoe sasa kama anataka, kwa sababu alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” 44Na wale wanyang’anyi waliokuwa wamesulibiwa pamoja naye pia walisema maneno ya kumdhihaki.

45Sasa kutoka saa sita kulikuwa na giza katika nchi yote hadi saa tisa. 46Ilipofika saa tisa, Yesu akalia kwa sauti kuu, “Eloi, Eloi, lama thabakithan?” akimaanisha, “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?” 47Wakati huo baadhi yao waliokuwa wamesimama pale walisikia, wakasema, “Anamwita Eliya.”

48Mara moja mmoja wao alikimbia kuchukua sifongo na kuijaza kinywaji kichungu, akaiweka juu ya mti na kumpa apate kunywa. 49Nao waliosalia wakasema, “Mwacheni peke yake, acheni tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.” 50Kisha Yesu akalia tena kwa sauti kuu na akaitoa roho yake.

51Tazama, Pazia la hekalu lilipasuka sehemu mbili kutokea juu hadi chini. Na ardhi ikatetemeka na miamba ikapasuka vipande. 52Makaburi yalifunguka, na miili ya watakatifu wengi waliokuwa wamelala usingizi walifufuliwa. 53Walitoka kwenye makaburi baada ya ufufuo wake, waliingia mji mtakatifu, na wakaonekana na wengi.

54Basi yule akida na wale ambao walikuwa wakimtazama Yesu waliona tetemeko na mambo yaliyokuwa yakitokea, walijawa na woga sana na kusema, “Kweli huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” 55Wanawake wengi waliokuwa wakimfuata Yesu kutoka Galilaya ili kumhudumia walikuwa pale wakitazama kutoka kwa mbali. 56Miongini mwao walikuwa Mariamu Magdarena, Mariamu mama yake Yakobo na Joseph, na mama wa watoto wa Zebedayo

57Ilipofika jioni, alikuja mtu tajiri kutoka Arimathayo, aliyeitwa Yusufu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. 58Alimwendea Pilato na kuuomba mwili wa Yesu. Kisha Pilato aliagiza apate kupewa.

59Yusufu aliuchukua mwili akaufunga na nguo ya sufi safi, 60na akaulaza katika kaburi jipya lake alilokuwa amelichonga mwambani. Kisha akavingirisha jiwe kubwa likafunika mlango wa kaburi na akaenda zake. 61Mariamu Magdalena na Mariamu mwingine walikuwa pale, wamekaa kuelekea kaburi.

62Siku iliyofuata ambayo ilikuwa siku baada ya maandalio, wakuu wa makuhani na Mafarisayo walikusanyika pamoja kwa Pilato. 63Wakamwambia, “Bwana, tunakumbuka kuwa wakati yule mdanganyifu alipokuwa hai, alisema, ‘Baada ya siku tatu atafufuka tena.’ 64Kwahiyo, agiza kwamba kaburi lilindwe salama mpaka siku ya tatu. Vinginevyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kumwiba na kusema kwa watu, ‘Amefufuka kutoka wafu.’ Na udanganyifu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”

65Pilato akawaambia, “Chukueni walinzi. Nendeni mkafanye hali ya usalama kama muwezavyo.” Hivyo walikwenda na kufanya kaburi kuwa salama, jiwe liligongwa mhuri na kuweka walinzi.

66

Copyright information for SwaULB